Watatu mbaroni kwa kusafirisha dawa za kulevya


DAR ES SALAAM: WAKAZI watatu wa Kigamboni mkoani Dar es Salaam wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin yenye uzito wa kilogramu 882.71 na Methamphetamine yenye uzito wa kilogramu 2167.29.


Washitakiwa hao ni mfanyabiashara Najim Mohamed (52), mfanyabiashara Maryam Mohamed (50) na Msaidizi wa kazi za ndani, Juma Abbas (37).


Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka na Wakili wa serikali mwandamizi, Hemed Halfan mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Aaron Lyamuya.


Halfan alidai kuwa katika shtaka la kwanza inadaiwa kuwa Desemba 15, 2023 washtakiwa wote wakiwa katika eneo la Kibugumo  shule lililopo Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam walikutwa wakisafirisha dawa ya kulevya aina ya Heroin yenye uzito wa kilogramu 882.71.


Katika shtaka la pili alidai kuwa katika eneo hilo na siku hiyo washtakiwa hao walikutwa wakisafirisha dawa ya kulevya aina ya Methamphetamine yenye uzito wa kilogramu 2167. 29.


Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka yanayowakabili, Hakimu Lyamuya alisema Mahakamani hiyo haina mamlaka ya  kusikiliza kesi hiyo hivyo washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote hadi watakavyoitwa Mahakamani Kuu.


Hata hivyo Wakili Halfan alidai kuwa upelelezi wa kesi bado haujakamilika na kuiomba Mahakama hiyo tarehe nyingine kwa ajili kutwaja.


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 11, 2024 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wote walirudishwa rumande baada ya kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE