Hoja kupinga mkataba wa bandari kuchambuliwa leo mahakamani

 Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya leo Jumatano Julai 26, 2023 inaanza rasmi kusikiliza kesi ya makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA) yanayohusha uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam kupitia kampuni ya Dubai Ports World (DP World).



Jana Julai 25, 2023, mawakili wa pande zote na Mahakama walikubaliana mambo sita kama viini vikuu vya kesi hiyo ambavyo mahakama inapaswa kuvitolea uamuzi.


Leo Julai 26, 2023, upande wa madai unaanza kuchambua viini hivyo kuthibitisha madai yao ya ubovu wa masharti ya makubaliano hayo, wakati wadaiwa watakuwa na kibarua cha kupangua hoja hizo kuonyesha kwamba masharti ya makubaliano hayo yako sawa na yamezingatia maslahi ya Taifa.


Kumekuwa na hoja nyingi kwenye mitandao ya kijamii, vijiweni na katika majukwaa ya kisiasa, mtu mmoja mmoja, makundi na au taasisi zinazosigana katika makubaliano hayo, huku kila upande ukijitahidi kuushawishi umma kuamini mtazamo wake.


Hata hivyo, hoja zinazotolewa leo ndizo rasmi zitakazowekwa kwenye kumbukumbu ya kudumu na ndizo zitakazoamua hatima ya makubaliano hayo.


Mawakili wa pande zote watachuana vikali kuonesha umahiri wa kujenga hoja na kutafsiri sheria na Katiba ili kuishawishi Mahakama kutoa uamuzi unaounga mkono moja ya pande hizo.


Tayari ukumbi umeshajaa watu, wakiwemo mawakili wa pande zote na wasikilizaji, wananchi wa kada na rika tofauti.


Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya na mawakili wanne kutoka mikoa tofauti, ambao ni Alphonce Lusako, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalus dhidi ya Serikali


Wadaiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye ni mshauri wa Serikali kwa masuala ya kisheria, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge la Tanzania, ambaye ni mtendaji mkuu na mratibu wa shughuli za Bunge.


Viini vya kesi hiyo vinavyopaswa kuamuriwa kuwa ni:


Mosi, kama kusaini, kuwasilisha bungeni na kuridhia mkataba waTanzania na Dubai kulikiuka kifungu cha 11 (1) na (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Rasilimali na Maliasili namba 5 ya mwaka 2017, na kifungu cha 5(1), 6(2) (a), (b), (e) na (i) cha Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba inayohousu Rasilimali na Maliasili za Nchi namba 6 ya mwaka 2017.


Mbili, kama umma uliarifiwa na kupewa muda muafaka kushiriki na kutoa maoni yao kama ambavyo sheria zinataka kuhusiana na utaratibu wa kupitisha na kuridhia Mikataba.


Tatu, kama ibara ya 2(1), 4(2), 5(1),  6(2), 7(2), 8(1) (a-c), (2); 10(1) , 20(2) (a), (e) na (i) na (ii); 18, 21, 23(1) (3) na (4); 26, 27, na 30(2) za mkataba huo zinakiuka ibara za 1, 8, 28(1) na (3) za Katiba ya Nchi.


Nne, Kama IGA (makubaliano hayo yaliyosainiwa) ni mkataba.


Tano, kama Ibara ya 2 na 23 ya mkataba huo zinakiuka kifungu cha 25 cha Sheria za Mikataba Tanzania.


Sita, kama IGA (makubaliano) kati ya Tanzania na Dubai ilifuata taratibu za kisheria katika kuchagua njia ya manunuzi ambao umewekwa chini ya kifungu cha 64 cha Sheria ya Manunuzi.


Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Dunstan Ndunguru. Wengine ni Mustafa Ismail na Abdi Kagomba.


Katika kesi hiyo ya kikatiba namba 5 ya mwaka 2023, wanasheria hao vijana wanapinga makubaliano hayo wakidai kuwa ni batili kwa kuwa masharti ya baadhi ya ibara zake yanakiuka Sheria za Nchi za Ulinzi wa Raslimali na Maliasili za Nchi na Katiba ya Nchi.


Vile vile wanadai kwamba yanahatarisha mamlaka ya Nchi na Usalama wa Taifa na kwamba yaliridhiwa na Bunge kinyume cha utaratibu bila kuwapa nafasi ya kutosha wananchi kutoa maoni yao.


Makubaliano hayo yalisainiwa Oktoba 25, 2022 na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, baada ya kupewa nguvu ya kisheria na Rais Samia Suluhu Hassan, huku Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, akishuhudia na yaliridhiwa na Bunge Juni 10, 2023.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE