Wabunge Walalamikia Visa Vya Watu Kutoweka

 NA COLLINS OMULO



KUNDI la wabunge kutoka Kaskazini Mashariki mwa Kenya, limelalamikia ongezeko la visa vya watu kutoka eneo hilo kutoweka kwa njia ya kutatanisha.


Wakiongozwa na Mbunge wa Garissa Mjini, Bw Dekow Mohamed na mwenzake wa Lagdera, Bw Mohamed Abdikadir, walielezea kughadhabishwa na kurejea kwa visa vya watu kupotea, kisa cha hivi punde kikiwa cha Sheikh Billow Abdi.


Wakiongea na wanahabari jijini Nairobi, Bw Mohamed alisema, Bw Abdi, 35, anayetoka kaunti ya Garissa, alipotea kwa njia isiyoeleweka mnamo Desemba 14, 2023, katika eneo la Kilimani, Nairobi.


Tangu wakati huo, familia ya mwalimu huyo wa masuala ya dini ya Kiislamu imefuata njia zote ikiwemo kuenda katika afisi husika za serikali, hospitali, vyumba vya kuhifadhi maiti wakimsaka bila mafanikio.


Bw Mohamed ambaye ni mbunge wa UDA, alisema kupotea kwa Bw Abdi ni kisa cha nne cha mtu kutoka eneo bunge la Garissa Mjini kutoweka bila kupatikana.


Hii ni licha ya visa hivyo kuripotiwa kwa vikosi vya usalama na hatua kutochukuliwa.


Visa hivyo, vimeongezeka licha ya Rais William Ruto kuahidi kuwa visa vya watu kupotea, kutekwa nyara na kuuawa kiholela havitashuhudiwa chini ya utawala wake.


“Kama viongozi tunashangazwa na kughadhabishwa na ongezeko la visa vya watu kutoka Kaskazini Mashariki mwa Kenya kupotea kwa njia za kutatanisha.


Hili ni suala ambalo Rais aliwahi kulizungumzia na kusema kuwa enzi za watu kupotea, kutekwa nyara na kuuawa kiholela zimeisha,” akasema Bw Mohamed.


“Inasikitisha kuwa tunakumbwa na hali kama hii tena. Ikiwa visa hivi vinahusishwa na vita dhidi ya ugaidi, utaratibu wa kisheria unapasa kufuatwa,” akaongeza.


Bw Mohamed alisema wao kama viongozi kutoka Kaskazini Mashariki mwa Kenya, wanaunga mkono juhudi za serikali kupambana na ugaidi lakini sharti sheria ifuatwe.


“Ikiwa maafisa wa usalama wamehusishwa na kutoweka kwa Bw Abdi, tunatarajia kuwa utaratibu wa sheria utafuatwa. Ikiwa polisi hawahusiki, basi tunawauliza maafisa wa usalama watueleze kilichomtendekea Abdi kwa sababu ni wajibu wao kulinda raia wa nchi hii,” akasema.


Kwa upande wake, Bw Abdikadir alisema kuwa visa vya watu kutoweka vimekithiri zaidi ndani ya muda wa miezi mitatu iliyopita.


Alisema ikiwa Bw Abdi alihusika katika visa vyovyote vya utovu wa usalama, basi serikali inapasa kumfikisha kortini.


Credit : Taifa Leo

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE