Mvutano Serikali, kanisa wachukua sura mpya Mbeya

 Waumini wa Kanisa la The Children of Gospel for All Nations (TCH-GOFAN) lililopo Wilaya ya Mbeya wamesema endapo Serikali wilayani hapa haitatoa kibali cha ujenzi wa kanisa lao watamchangia mchungaji wao kwenda kumuona Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kuingilia kati.



Hatua hiyo imekuja kufuatia kuwepo kwa mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 20, baada ya Serikali kuweka zuio la uendelezaji wa makazi na kanisa katika Bonde la Ilolo, ambalo linaelezwa kuwa kwenye mkondo wa maji.


Akizungumza na waandishi habari leo, Jumapili Desemba 24, 2023, Mchungaji kiongozi wa Makanisa ya TCH-GOFAN, John Ikowelo amesema wamevumilia kwa takribani miaka 20 lakini hawajui hatima yao, licha ya kufuatilia hatua kwa hatua kwa viongozi wa Serikali, akiwemo mkuu wa wilaya hiyo.


“Hilo eneo lipo jirani na Shule ya Msingi Isanga, ni mali ya kanisa lakini cha kushangaza baada ya mgogoro ya awali kuisha, wakati tumeanza kumwaga mawe, mchanga na hatua za kuchimba msingi tumeletewa barua ya kuwekewa zuio,” amesema.


Mchungaji Ikowelo amesema hatua hiyo imewashangaza, licha ya kuwa wavumilivu na kutumia busara, hivyo amewataka viongozi wa Serikali kuwa hofu ya Mungu kwa kutenda haki.


Amesema kwa sasa hawako tayari kuendelea kupoteza muda, wanasubiri kauli ya mwisho ya mkuu wa wilaya ili kuchukua hatua ya kwenda kuonana na Rais Samia.


“Tumechoka kuzungushwa, kama kanisa tulitumia busara kuanzia ngazi za chini za viongozi wa Serikali lakini hawaoni hilo, si kwamba tumeshindwa kumuona Mbunge Dk Tulia Ackson na Mkuu wa Mkoa, Juma Homera ila hatutaki kuwatwisha mzigo ambao umeshindwa kutatuliwa na watu walio chini yao,” amesema.


Mmoja wa waumini wa kanisa hilo, Enelise Kyanula amesema waumini walichanga mawe, mchanga na nguvu kazi kwa ajili ya kuanza ujenzi lakini cha kushangaza wameletewa barua ya zuio.


“Kwa sasa tumefika wakati tumechoka tunaendelea kuomba na kulia tu, kinachofuata ni kujichanga ili kiongozi wa kanisa akaonane na Rais Samia aweze kuingilia kati haki itendeke, tujenge nyumba ya bwana,” amesema.


Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amesema kama Serikali haitaweza kutoa kibali cha ujenzi kwa sababu ni eneo oevu, eneo hilo halitaruhusiwa kuwekezwa mradi wowote.


“Nilipofika Mbeya nimeukuta mgogoro huo, nimefika eneo linalolalamikiwa nimeongea na viongozi wa kanisa, kimsingi nimepewa maelezo na Mkurugenzi wa Jiji na watu wa ardhi kuwa halistahili kujengwa kwa sababu ni oevu,”amesema Malisa.


Amesema kuwa kama Serikali sasa wanaangalia ni wapi halmashauri itapata eneo la wazi na kulikabidhi kanisa hilo kwa ajili ya ujenzi.


Kuhusu kuwekeza pale, haitowezekana na endapo hawataridhia, waendelee na hatua nyingine kama vile kwenda mahakamani.


0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE