Mgogoro wachimbaji Simiyu wapata ufumbuzi

 Simiyu. Hatimaye mgogoro kati ya Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (Tawoma) na Emmanuel Silanga kuhusu eneo la uchimbaji madini mkoani Simiyu, umemalizika.



Hatua hiyo imetokana na Serikali mkoani humo kuingilia kati na kuamua umiliki wa mgodi huo uwe kwa ubia kati ya Tawoma na Silanga.


Awali, ilidaiwa chanzo cha mgogoro huo ni mapato yanayotokana na shughuli za uchimbaji kwenye mgodi wa Dutwa namba 10 ambao Silanga ndiye mwenye leseni halali.


Hata hivyo, imeelezwa Tawoma walikuwa wakiendesha shughuli zao kwenye mgodi huo, huku wakidai sehemu ya mrabaha licha ya kutokuwa na umiliki.


Akizungumza jana Desemba 25,2023 baada ya kutatua mgogoro huo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda amesema kuanzia sasa shughuli zote za uendeshaji wa leseni ya mgodi huo zitafanywa kwa ubia.


“Kuanzia Jumatatu tumekubaliana shughuli zote za usimamizi zitafanywa na kina mama hawa, ninachowaomba kama kukiwa na jambo lingine fikeni Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,” amesema.


Ameeleza dhamira ya uamuzi huo ni kuhakikisha maslahi ya pande zote yanapatikana, kwa kuwa wote wanalipa kodi na ushuru serikalini.


“Mkianza tena mambo ya sintofahamu mrudi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, wala msiite vyombo vya habari, ili tumalize mgogoro, nilitumwa na chama changu (CCM) nimalize tatizo hili na nashukuru nimemaliza,” amesema.


Mmiliki mwenza wa mgodi huo, Silanga amesema haukuwa mgogoro mkubwa, isipokuwa ulichagizwa na hatua ya usikilizwaji kufanyika kwa upande mmoja.


Hata hivyo, amewataka Tawoma kuacha kuwasikiliza baadhi ya wanasiasa, ili kuepuka kuichafua taswira ya Mkoa wa Simiyu.


“Hawa kina mama wasitumiwe na wanasiasa wanaoweza kuharibu taswira ya Simiyu, kina mama mimi nawapenda kwa sababu mimi ni baba natakiwa niwatunze, nao watutunze.


“Haukuwa mgogoro, ilikuwa ni lugha gongana lakini dhamira yetu ni kuwaendeleza kina mama na hilo tunaunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan. Kwa hiyo mimi nitakuwa napata ripoti kutoka kwa wakina mama,” amesema.


Naye Mwenyekiti wa Tawoma, Nimeri Chacha amesema wamepitia magumu mengi, lakini mkuu wa mkoa na viongozi wa CCM wamepambana kuwafikisha katika hatua hiyo.


“Wametupigania hatimaye leo tumekuja kupata haki yetu, tunashukuru sana CCM Mkoa huu wa Simiyu,” amesema.


0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE