Mabasi matano yazuiliwa kuendeleza na safari Mbeya

 Mbeya. Jeshi la Polisi nchini limeyazuia mabasi matano yanayofanya safari za mikoani baada ya kufanya ukaguzi na kubaini yana hitilafu za mifumo.



 Katika ukaguzi huo uliofanyika leo Jumanne Desemba 26, 2023 katika kituo kikuu cha mabasi ya mikoani jijini hapa, mabasi yaliyositishiwa safari ni kutoka kampuni za Turu Best, Isamilo Express, Arusha Express, Msigwa na Ahmed.


Mbali na kusitishiwa safari madereva pia walipimwa ulevi.



Mwanasheria Mkuu wa Kikosi cha usalama Barabarani, Mrakibu mwandamizi wa Polisi, Deus Sokoni, amesema ukaguzi huo umelenga kudhibiti ajali na kutoa elimu.


“Mabasi ya abiria 58 yamekaguliwa kati ya hayo matano kutoka kampeni ya Turu  best, Isamilo Express, Arusha Express, Msingwa na Ahmed yamesitishwa kuendelea na safari mpaka yafanyiwe marekebisho ili kulinda usalama wa abiria,”amesema.


Amesema Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana na mamlaka nyingine ikiwepo Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), wamepewa idhini ya kuzuia chombo cha moto kuendelea na safari pindi wanapofanya ukaguzi na kugundua ubovu au hitilafu katika mifumo ya chombo hicho.


Kwa upande wake Ofisa Leseni Latra, Amani Masuwe amesema wamefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha abiria waliokuwa wasafiri na mabasi hayo wanapata usafiri mwingine na wengine kurudishiwa nauli zao, ili kufanya utaratibu wa safari kwa siku nyingine.


Naye Balozi wa usalama barabarani Mkoa wa Mbeya, Yonna Mleka amewataka madereva kujenga utamaduni wa kufanya ukaguzi wa magari yao kabla ya kuanza safari ili kuepuka usumbufu kwao na kwa abiria wanaowasafirisha na kuepuka madhara mengine wawapo safarini.


Ameongeza kuwa, mabalozi wa usalama barabarani wataendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa elimu kwa abiria kupitia kampeni ya Abiria Paza Sauti (APS).


0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE