Kihenzile akabidhi vifaa tiba vya Sh bilioni 1.8 hospitali Mufindi

 HOSPITALI ya Wilaya ya Mufindi imepokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh Bilioni 1.8 kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini, David Kihenzile aliyeahidi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2020 kushirikiana na wadau wake mbalimbali kuboresha huduma za afya wilayani humo.



Kihenzile ambaye pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi amesema kwa kupitia nafasi yake ya uwakilishi wa wananchi, moja ya wajibu wake ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha huduma za afya na ustawi wa jamii.


Akikabidhi kontena zima lenye vifaa hivyo mbele ya Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Jimbo la Mufindi Kusini, Naibu Waziri huyo amezungumzia umuhimu wa vifaa tiba akisema ni sehemu muhimu ya mchakato wa tiba na husaidia wataalamu wa afya kufanya maamuzi sahihi na kutoa matibabu yenye ufanisi.


Alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan akisema kazi yake ya kuimarisha sekta ya afya na nyingine za maendeleo ni ya kutukuka inayolenga kuhakikisha wananchi wakiwemo wenye kipato duni wanapata huduma kwa urahisi.

“Mheshimiwa Rais anajali sana afya za wananchi na ndio maana hasiti kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha na kusogeza huduma kwa wananchi. Sisi kama wasaidizi wake tutahakikisha tunaunga mkono juhudi hizo ili kuboresha maisha ya Watanzania,” alisema.


Kihenzile alisema msaada huo mkubwa wa vifaa tiba wilayani humo ni wa pili baada ya ule wa thamani ya Sh Bilioni 1.5 alioutoa mwaka 2021.


‘’Ndugu wananchi na viongozi wa chama, huu ni msaada wa pili hii wa vifaa tiba mbalimbali unaofanya thamani ya misaada yote miwili tuliyotoa kuwa zaidi ya Sh Bilioni 3. Ninawaahidi nitaendelea kushirikiana nanyi kusukuma gurudumu la maendeleo ya wananchi wetu na kutatua changamoto zao,’’alisema.


Katika hatua nyingine Mbunge Kihenzile amewataka watumishi wa kada ya afya waliopo kwenye Jimbo lake la Mufindi Kusini kufanya kazi kwa weledi ili kuendana na kasi ya Rais katika utoaji huduma bora kwa wananchi.


‘’Natoa rai kwa watumishi wote wa afya kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia taaluma yenu na weledi na atakayebainika anakwamisha juhudi za serikali tutamuodoa haraka,’’ alisema.


Kwa upande wake Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mkuu wa Idara ya Organaizesheni, Issa Gavu aliwasihi wananchi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita katika kuboresha sekta mbalimbali za huduma nchini.


Gavu aliwataka viongozi waliopewa dhamana kuhakikisha wanamsaidia Rais kueleza kwa wananchi yale yote yanayotekelezwa na serikali katika maeneo yao.


Akipokea vifaa hivyo Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi Dk Fredrick Jackorache alimshukuru Kihenzile kwa mchango huo akisema utaleta nafuu katika utoaji wa huduma katika hospitali hiyo kwa kupunguza vikwazo katika utoaji wa huduma za afya na kuathiri ufanisi wa matibabu.


Mwisho.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE