Kairuki kuwafungulia fursa wanakilimanjaro

 

KILIMANJARO: WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Angela Kairuki anatarajia kuzindua programu maalum ya ‘Homestay’ inayotoa fursa kwa wananchi wa Kilimanjaro kujisajili na kuruhusu nyumba zao zitumike kwa malazi ya wageni watakaofika kwa shughuli mbalimbali za utalii na kutembelea vivutio vilivyopo mkoani Kilimanjaro.


Kairuki anatarajiwa kuzindua programu hiyo kesho kutwa Alhamisi katika tamasha la Kilimanjaro Cultural Festival (KCF) litakafanyika kesho na keshokutwa mkoani Kilimanjaro.


Mwenyekiti wa KCF, Ansi Mmasi amesema hayo katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari leo.


Mmasi amesema mbali na Kairuki kuzindua programu hiyo, atakabidhi zawadi kwa vikundi vya washindi wa ngoma za asili na watoto wa umri wa kati ya miaka 16 hadi 18 waliofanya vizuri kwenye shindano la kuzungumzia vivutio vya asili katika maeneo yao kwa lugha fasaha za asili za makabila yao.


Amesema katika siku ya kwanza ya tamasha yaani kesho, Mkuu wa Mkoa huo Nurdin Babu ndiye atakayelifungua, kisha timu ya msafara wake itatembelea mapango ya asili ya Chagga curve yaliyopo Marangu na msafara mwingine utaelekea Kibosho Kirima kutembelea mapango ya asili ya Nubi curve.


Amesema kwa kuwa mkoa huo una vivutio vingi sio rahisi kuvimaliza vyote kwa siku moja, hivyo uwepo wa tamasha hilo ni sehemu ya kufungua njia kwa wanakilimanjaro, watanzania wote na wageni kutembelea vivutio mbalimbali vikiwemo vya asili vilivyopo maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kilimanjaro.


Amewaasa wana Kilimanjaro kutumia tamasha hilo kujifunza, kushauri na kuboresha zaidi ili matamasha mengine ya aina hiyo yaendelee kuleta tija kwa wana jamii wa Kilimanjaro.


“Fikeni kujionea ngoma za asili, vyakula na vinywaji vya asili kama Kirembwe, ugali wa ndizi, Ikatwe, ngararimu, ndizi choma za magadi, mbege, dengerua,kitalolo cha maziwa,kitawa,kiburu nk, mle, mnywe lakini muone ngoma za makabila ya asili ya wachaga, wapare na wamasai na mambo mengi mazuri,” amesema.


Amesema katika tamasha hilo hakuna kiingilio chochote hivyo wachopaswa ni kujitokeza kwa wingi eneo hilo la Kilihome kwa ajili ya kushuhudia mambo mbalimbali zikiwemo mila, tamaduni na desturi pamoja na kufahamu vivutio vya asili vilivyopo Kilimanjaro.


KCF ni asasi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa kupitia mawazo ya kundi sogozi la WhatsApp la wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wanaoishi ndani na nje ya mkoa huo, baada ya kukutana ana kwa ana mwaka 2019 na kushauriana kutumia nafasi hiyo kuwa na kitu chenye mlengo chanya wa maendeleo ya kusaidia jamii ya wanakilimanjaro na taifa kwa ujumla.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE