Chadema yafunguka uamuzi wa Mahakama kuhusu kina Mdee

 Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema, kinautafakari uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kutengua uamuzi wa Baraza Kuu la chama hicho dhidi ya waliokuwa wanachama wake 19 akiwamo Halima Mdee.



 Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi, Desemba 14, 2023 na Jaji Cyprian Mheka ambaye amesema kitendo cha wajumbe wa Kamati Kuu kuwa pia wajumbe wa Baraza Kuu na kutoa uamuzi wa rufaa ni kinyume cha kanuni za haki asili.


Pia, Mahakama imeitaka Chadema kuzingatia haki za asili wakati ikishughulikia rufaa za Mdee na wenzake 18.


Baada ya uamuzi huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema ametoa taarifa kwa umma akisema wanautafakari uamuzi ikiwamo kumkumbusha Spika wa Bunge.


“Kwa uamuzi wa kuwafukuza uanachama waliokuwa wanachama wetu 19 uliofanywa na Kamati Kuu ya chama, umeendelea kusimama (upo palepale) na Mahakama imekubaliana taratibu zote za katiba ya Chadema na sheria za nchi zilifuatwa kikamilifu na Kamati Kuu katika kuchukua uamuzi huo,” amesema Mrema.


Mrema amesema uamuzi wa Baraza Kuu kuhusu rufaa umefutwa, hivyo Baraza Kuu linapaswa kukaa upya kusikiliza rufaa hiyo; lakini Kamati Kuu ilishawafukuza uanachama na uamuzi wake jaji upo sahihi.


“Hivyo basi, kwa hatua ya sasa chama kitawasiliana na mawakili wake ili kutafakari hatua za kuchukua ikiwa ni pamoja na kumkumbusha Spika wa Bunge kuhusu utekelezaji wa uamuzi wa Kamati Kuu ya Novemba 27, 2020 kwani Mahakama imethibitisha walifukuzwa uanachama kihalali na taratibu zote zilifuatwa,” amesema Mrema 


Mbali na Mdee, aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha), wengine waliofukuzwa Chadema, ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu (CC), Esther Matiko na Ester Bulaya; aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara), Hawa Subira Mwaifunga na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.


Wengine, ni aliyekuwa Katibu mkuu wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), Nusrat Hanje; aliyekuwa Naibu katibu mkuu wa Bawacha (Bara), Jesca David Kishoa; Cecilia Pareso, Agnesta Lambart, ambaye alikuwa mwenezi wa Bawacha na Tunza Malapa, aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, mkoani Mtwara.


Katika orodha hiyo, wamo pia Asia Mohammed, aliyekuwa Naibu Katibu mkuu wa Bawacha (Zanzibar), Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.


0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE