CCM yataka wananchi washiriki marekebisho sheria za uchaguzi

 

WANANCHI wametakiwa kushiriki marekebisho ya sheria za uchaguzi, kwa kuwasilisha mapendekezo yao bungeni jijini Dodoma, kwa ajili ya maboresho ya miswada ya sheria hizo iliyowasilishwa na serikali hivi karibuni. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).


Wito huo umetolewa leo tarehe 21 Disemba 2023, jijini Dar es Salaam na Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Paul Makonda, akizungumza na waandishi wa habari.


“Serikali imepeleka muswada bungeni ya mabadiliko ya sheria na sasa Bunge limetoa tangazo kuruhusu wananchi wote kushiriki katika kutoa mapendekezo wanataka sheria hizi zinazohusu mambo kadhaa wa kadhaa ikiwemo ya uchaguzi, tume ya uchaguzi na vyama vya siasa,” amesema Makonda na kuongeza:


“Katika jambo hili chama tumeweka mkazo kwamba hiki kipindi cha kutoa maoni, kinatoa rai kwa wananchi washiriki kikamilifu katika kutoa maoni kwa tangazo la Bunge ili mapendekezo haya ya muswada yatakapofika kutengeneza sheria ili wananchi wawe wameshiriki kikamilifu.”


Mnamo tarehe 10 Novemba mwaka huu, Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, pamoja na wa marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, ilisomwa kwa mara ya kwanza bungeni jijini Dodoma.


Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, umewasilishwa kwa lengo la kubainisha muundo, majukumu, utaratibu wa upatikanaji wajumbe wa tume, sifa za mkurugenzi wa uchaguzi na mambo mengine yanayohusiana na tume hiyo.


Kuhusu Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa, umewasilishwa kwa lengo la kuimarisha nafasi ya msajili wa vyama vya siasa kama msimamizi wa mienendo ya vyama pamoja na kuimarisha uzingatiaji wa sheria na kanuni katika vyama hivyo.


Tangu miswada hiyo iwasilishwe bungeni, baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani ikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeikosoa ikitaka iondolewe bungeni ili Serikali ikaifanyie marekebisho kikidai haijalenga kutatua changamoto za mfumo wa uchaguzi zinazolalamikiwa na wadau.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE