Barua ya Mdee, wenzake zilifanana hadi nukta na koma

 Jana tuliwaletea mawasilisho (final submissions) za mawakili wa wajibu maombi ambao ni Halima Mdee na wenzake 18, leo tunaendelea na mawasilisho ya upande wa wajibu maombi, ambao ni Baraza la Wadhamini wa Chadema.



Wajibu katika wasilisho lao kwa mujibu wa jaji, walieleza kuwa hakuna rejea mahsusi iliyowasilishwa na waleta maombi ikionyesha kwamba waleta maombi hao pia walikuwa wanapinga uamuzi wa Kamati Kuu wa Novemba 27, 2020.


Mawakili wa wajibu maombi waliyapinga malalamiko ya msingi ya akina Mdee na wenzake kwamba Kamati Kuu haikuwapa haki kamili ya kusikilizwa au kwamba mkutano wa Baraza Kuu ulikuwa na upendeleo au ulikuwa na ushawishi.



Jaji Mkeha alisema wajibu maombi walisema kutokana na ukweli kuwa Mdee na wenzake walikiri kupokea wito kwa njia ambayo inakubaliwa na katiba yao wenyewe, walipoamua kutohudhuria maamuzi yasingekuwa na faida kwao.


“Mjibu maombi wa kwanza anasema nafasi ambayo walitakiwa kuwapa na ambayo waliwapa ni haki ya kusikilizwa,” alieleza Jaji Mkeha.


Katika wasilisho lao waliegemea kesi ya Pantaleo Lyakurwa dhidi ya Leokadia Lyakurwa ya mwaka 1998, iliyoweka msimamo kuwa kanuni dhidi ya upendeleo haiondoi haki ya kufanya uamuzi wa upande mmoja, kama mhusika aliamua kutohudhuria.


“Waliwasilisha kuwa upande ambao ulipewa wito kikamilifu wa kikao cha usikilizwaji, halafu ukaamua wenyewe kutohudhuria unachukuliwa kama walijiondolea wenyewe haki ya kusikilizwa,” alieleza Jaji Mkeha na kuongeza;


“Wakasisitiza ingawa ilielekezwa wahudhurie kikao hicho, kwa yeyote aliyekuwa anafanya jambo kwa nia njema angeweza kutuma hata mwakilishi, lakini kwa kuamua kutohudhuria kuliwaondolea haki ya kusikilizwa na kamati kuu.”


Mjibu maombi akaeleza kuwa ilikuwa ni jambo la kushangaza kwamba inawezekanaje waombaji wote 19 kukataa au kudharau kuhudhuria kamati kuu wakiwa na sababu zinazofanana hadi alama ya koma na nukta kupitia barua zao.


Hiyo, kwa mujibu wa Baraza la Wadhamini la Chadema, ilikuwa haina maana nyingine zaidi ya kwamba ulikuwa ni mkakati rahisi wa waleta maombi hao 19.

 


Hakukuwa na kitisho cha usalama


Katika wasilisho lao la mwisho, mawakili wa wajibu maombi kulikuwa hakuna ushahidi wowote wa kuwepo kitisho cha usalama kwa Mdee na wenzake na kwamba mtu mmoja kubeba bango la kuwalaani, halikuwa na maana ni kitisho.


Pia walieleza kuwa licha ya kutokuwepo ushahidi wowote wa kuwepo tishio la usalama kwa waleta maombi, kamati kuu tena kwa gharama kubwa na changamoto, ilihamishia mkutano Ledger Plaza Bahari Beach, ili kuondoa hofu.


“Mawakili wa wajibu maombi wanasema walishangaa kwamba kama kweli kulikuwa na tishio la usalama, haikuripotiwa kituo chochote cha polisi”.


Katika kujibu hoja ya waleta maombi kuwa kamati kuu iliongeza madai mengine ambayo hayakuwemo kwenye barua ya wito, mawakili wa wajibu maombi walishikilia msimamo kuwa wakati wote tuhuma zao zilibaki zile zile.


Tuhuma hizo zilikuwa ni kwamba wote 19 walijitwisha nafasi ya viti maalumu bungeni kwa kuonyesha walidhaminiwa na Chadema, bila kuzingatia mchakato ndani ya chama na wakakiuka msimamo wa chama kuhusu uchaguzi wa 2020.

 


Kauli za John Mnyika


Mawakili hao waliendelea kuwasilisha kuwa matamshi ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika katika mkutano na wanahabari kuelekea kikao cha kamati kuu yalishatoa ni uamuzi gani unakwenda kufanyika ni udanganyifu.


“Kulingana na mawakili hao, yale aliyoyafanya katibu mkuu ilikuwa ni kuwaita waombaji wahudhurie kikao cha kamati kuu ili kutetea matendo yao ambayo Chadema waliyatafsiri kuwa ulikuwa ni usaliti wa misingi ya kisiasa,” alisema.

Jaji akaendelea kueleza kuwa kama mwanasiasa achague maneno ya kuzungumza kwa umakini kama vile jaji anavyofanya katika hotuba yake.


Ingawa waleta maombi waliegemea kifungu 6.5.1(a) cha Katiba ya Chadema kukosoa uamuzi wa kamati kuu kushindwa kuwapa notisi ya siku 14, kifungu 6.5.1(b) cha Katiba hiyo hiyo kilitoa ruhusa kushughulikia nidhamu kwa dharura.


Kuhusiana na uamuzi wa Baraza Kuu, mawakili hao walisema Mdee na wenzake walikuwa hawapingi uhalali, ufanisi au Katiba ya Chadema kwa sababu kuna njia tofauti za kupinga vifungu vya Katiba kama wangekuwa wanalalamikia Katiba.

“Muda wote walikuwa wanaifuata Katiba hiyo hadi mgogoro ulipojitokeza,” alisema Jaji Mkeha akinukuu wasilisho la mawakili wa wajibu maombi.

 


Wajumbe wa vikao viwili


Wakiwasilisha maoni juu ya hoja kuwa wajumbe wa Kamati kuu walishiriki Baraza Kuu la Rufaa, mawakili wa wajibu maombi walishikilia msimamo kuwa chini ya ibara ya 7.7.11, itaendelea kuwa hivyo hadi itakaporekebishwa au kupingwa kortini.


Kuhusiana na matamshi ya Mwenyekiti wa Taifa Chadema, aliyoyatoa kabla ya mkutano wa Baraza Kuu kwamba ni kama yalishatoa hukumu, mawakili hao walisema kiukweli walisikilizwa kikamilifu na kuwasilisha rufaa zao.


“Mawakili hao walieleza Chadema walienda mbali zaidi na kuwaita waombaji wote 19 kila mmoja kwa binafsi yake kuhudhuria kikao. Mchakato wa rufaa ulikuwa wazi kiasi hata cha kumwalika Naibu Msajili wa vyama, Sisty Nyahoza,” alisema Jaji.

Mawakili hao walieleza kuwa baada ya Baraza Kuu kuwa limeshatoa uamuzi wake Mei 11, 2022, ombi la kuzuia uamuzi wake lilikuwa halina maana tena.

 


Hoja za kuamuliwa na Mahakama


Baada ya kukamilika kwa mawasilisho hayo na ushahidi, Mahakama ilikuja na hoja tano ambazo ilisema zilihitaji kuamuliwa na Mahakama hiyo wakati wa kufanya uamuzi.


Hoja hizo ni kama Chadema, chini ya Katiba yake au kanuni, zinakipa nguvu au mamlaka ya kusikiliza kikao cha nidhamu katika mazingira ya dharura na kama jibu ni ndio, kama akina Mdee na wenzae walipewa haki ya kusikilizwa mbele ya Kamati Kuu.


Hoja nyingine ni kama walipewa haki ya kusikilizwa mbele ya Baraza Kuu ambacho ndio chombo cha rufaa, kama kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu, kama Baraza Kuu lilikiuka kanuni ya kutopendelea na kama maombi hayo yamekidhi vigezo vya kukubaliwa.


Kamati Kuu ya Chadema, iliwavua uanachama kwa madai ya kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu wakati kamati kuu ilikuwa haijafanya uteuzi wowote wa nafasi hizo kwa mujibu wa Ibara ya 7.7.16(a) ya Katiba ya chama hicho.


Halima Mdee na wenzake, walivuliwa uanachama wa chama hicho na Kamati Kuu ya Chadema, Novemba 27, 2020 wakakata rufaa Baraza Kuu la chama hicho ambalo liliketi Mei 11, 2022 kusikiliza rufaa na likabariki uamuzi wa Kamati Kuu.


Wengine waliovuliwa uanachama ni Grace Tendega, Ester Matiko, Ester Bulaya, Agnesta Kaiza, Anatropia Theonest, Asya Mohamed, Cecilia Paresso, Conchesta Rwamlaza, Felister Njau, Hawa Maifunga, Jesca Kishoa na Kunti Majala.


Katika orodha hiyo wamo Naghenjwa Kaboyoka, Nusrat Hanje, Salome Makamba, Sophia Mwakagenda, Stella Fiyao na Tunza Malapo na wote pamoja hawakuridhika na uamuzi wa Baraza Kuu kubariki uamuzi wa Kamati Kuu.


Hukumu hiyo ya Jaji Mkeha imekuwa na maoni na tafsiri tofauti miongoni mwa baadhi ya viongozi wa Chadema, wanachama na wafuasi wa chama hicho na kwa msingi huo, tunawaletea kwa usahihi nini hasa kilichomo katika hukumu hiyo.

Usikose kufuatilia mwendelezo wa simulizi ya hatua kwa hatua ya kesi hii kesho.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE