Ajali yaua wanane, chanzo mwendokasi na uzembe

 KIGOMA: WATU wanane waliokuwa wakisafiri na gari ndogo aina ya Probox Succeed maarufu kama mchomoko wamefariki dunia papo hapo na wengine sita wamejeruhiwa  baada ya gari waliyokuwa wakisafiri kugongana uso kwa  uso na  gari ya kampuni ya CHICCO inayotengeneza Barabara ya kiwango cha lami kutoka Kibondo mjini hadi Mabamba mpakani mwa Tanzania na Burundi.



Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari mjini Kigoma  amesema kuwa ajali hiyo imetokea Desemba 23 mwaka huu  majira ya saa 11 jioni katika Kijiji cha Kilemba Wilaya ya Kibondo ambapo gari hiyo ndogo ilikuwa ikifanya safari zake kati ya Kibondo na Kakonko.


Andengenye amesema kuwa hadi kufikia  asubuhi leo miili ya watu sita ilikuwa imetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao na kwamba hadi sasa miili ya watu wawili bado ipo Hospitali ya Wilaya Kibondo na watu wameombwa kufika hospitalini hapo kuitambua miili hiyo.


Waliofariki kwenye ajali hiyo wametajwa kuwa ni Pamoja na dereva wa gari ndogo, Hamisi Chaurembo (27), Bernadina Reuben  (22), Madua Asukile, Ntiganiza Bihezako (67), Vedastus Paul (28), Vladmir Vedastus (1) marehemu wengine wawili ambao majina yao hayajatambuliwa hadi sasa.


Akizungumzia majeruhi wa ajali hiyo Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa watu watatu wametibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani ambapo majeruhi watatu wameonakana kuhitaji matibabu zaidi, hivyo watahamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando Mwanza.


Waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo wametajwa kuwa ni dereva wa gari la CHICCO, Flavian Felishian (28) aliyejeruhiwa kichwani na kifuani, Juma Saidi (27), Daniel Samwel (33), Silvanus Muhigwa (43) Sara Bundala na Dori Mafumbo (22).


Mkuu huyo ametumia nafasi hiyo ya mkutano wake na waandishi wa habari kutoa pole kwa ndugu wa marehemu na kuwataka watu wote mkoani humo kuchukua tahadhari barabarani hasa wakati huu wa likizo ya mwisho wa mwaka ambao umekuwa na ongezeko kubwa kwenye vyombo vya usafiri.


Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Filemon Makungu ambaye alitembelea eneo la tukio alitaja gari zilizohusika na ajali hiyo kuwa ni T 833 DUA aina ya FAW mali ya kampuni ya CHICCO na gari ndogo aina ya Toyota SUCEED yenye namba za usajili T 890 DYZ mali ya Hamisi Chaurembo dereva wa gari aliyefariki kwenye ajali hiyo.


Kamanda Makungu amesema kuwa uchunguzi wa polisi umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na uzembe wa dereva wa dereva wa gari ndogo na ambaye alishindwa kulimudu gari hilo kwenye kona kali hivyo kugongana uso kwa uso na gari hilo la CHICCO.


Chanzo : Habari leo

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE