Mradi uchakataji gesi kuzalisha ajira 13,000

 

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitarajia kutiliana saini ya makubaliano ya mwisho kabla ya kuanza utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa uchakataji na usimikaji gesi asilia (LNG) wenye thamani ya Sh70 trilioni ifikapo Novemba mwaka huu, Watanzania 13,000 watanufaika na ajira mpya.



Juni 11, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya awali na kampuni kubwa za uchimbaji mafuta duniani, zikiwemo Equinor na Shell kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa uchakataji na usimikaji gesi asilia (LNG) wenye thamani ya Dola 30 za Marekani (wastani wa Sh70 trilioni).


Hayo yalisemwa juzi na Waziri wa Nishati, Januari Makamba alipokuwa akihojiwa katika kituo cha televisheni kupitia kipindi cha Clouds 360.


Alisema hiyo itakuwa fursa kwa Watanzania kwa kuwa mradi huo utatoa ajira za moja kwa moja 13,000 mpaka 16,000 na utaongeza mapato kwa Serikali.


Alisema wakati wa ujenzi kutahitajika nyumba za watu, maguta, ulinzi, bima, chakula, usafirishaji, mafundi kila nyanja ya uchumi wa nchi itaguswa na kikubwa maandalizi ya kwenye usambazaji.


Makamba alisema mradi utahitaji mafundi wa fani ya uchomeleaji wapatao 400 mpaka 600 kwa ajili ya kutengeneza mapipa makubwa ya kuhifadhi gesi, akisisitiza kuwa bado nchi haina mafundi wa aina hiyo. “Serikali tayari ina mpango wa kuanzisha chuo cha mafundi wa aina hii Lindi na jiwe la msingi la ujezi wa chuo hicho litawekwa na Rais, ifikapo Januari.


Alisema kuanza kwa mradi huo kutarahisisha mambo mengi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya usambazaji gesi maeneo mengi nchini licha ya nyingine kuuzwa nje ya nchi. “Watanzania walio wengi wanapenda kutumia vitu kidogo kidogo, Serikali ina mpango wa kuhakikisha kila nyumba inakuwa na mtungi wa gesi ya kupikia, teknolojia vumbuzi ya kuipima kidogo kidogo,” alisema Makamba.




Serikali yapitia upya mfumo wa umeme nchini


Katika hatua nyingine, Serikali imesema inaendelea na mapitio ya mpango mkuu wa mfumo wa umeme nchini, ili kuongezea miradi mipya iliyoongezeka.


Akizungumza jana katika kongamano la Taifa la mabadiliko ya tabianchi na nishati lililofanyika jijini hapa, likihusisha wadau wa nishati na mashirika yasiyo ya Serikali, Kamishna msaidizi wa Maendeleo ya umeme wa Wizara ya Nishati, Styden Rwebangila alisema mbali na mfumo huo, Serikali imejikita kwenye vyanzo vya umeme ili kuongeza upatikanaji.


“Tunatarajia ifikapo Juni 2023 utakuwa umekamilika. Mpango huu tumekuwa tukiuhuisha mara kwa mara kutokana na kuongezeka kwa vyanzo vipya vya umeme,” alisema Rwebangila.


Alisema hadi sasa Serikali imefikisha miundombinu ya umeme kwa asilimia 78.4, huku Watanzania waliounganishwa wakifikia asilimia 37.7.


Akizungumzia idadi ndogo ya Watanzania walioungwa na umeme katika kongamano hilo, Profesa wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Abel Kinyondo alisema suala la upatikanaji wa nishati linapaswa kuunganishwa na hali ya kipato cha wananchi.


“Licha ya bei ya umeme nchini kuwa chini kuliko nchi nyingine, baadhi ya Watanzania hawana uwezo wa kumudu gharama hizo, ndiyo maana wengine wamevuta umeme lakini maharage wanapikia mkaa kwa sababu tatizo ni kipato.


“Hivyo usambazaji wa umeme unatakiwa uende sambamba na ukuaji wa maendeleo ya watu,” alisema.


Nyongeza na Elias Msuya.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE