Familia Ya Mkenya Aliyekwama Guantanamo Yataka Ruto Aingilie Kati

 NA FARHIYA HUSSEIN



JAMAA za Mkenya mmoja anayezuiliwa katika gereza la Amerika la Guantanamo Bay nchini Cuba, imeomba serikali iwasaidie kumrejesha nyumbani mpendwa wao baada ya wakili Bw Miguna Miguna kurudi nchini.


Amerika haikumpata Bw Malik Mohammed Abdul na hatia na ikamwachilia huru mnamo Januari, lakini hajarejea nchini tangu wakati huo.


“Ni jana tu tumemuona Bw Miguna amerejea nchini baada ya kutimuliwa hapo awali, kudhalilishwa na kuteswa. Ombi langu ni Rais William Ruto kumrejesha ndugu yangu Bw Malik ambaye amekaa miaka mingi kule Guantanamo nchini Cuba,” alisema dadake Bw Abdul, Bi Mwajuma Rajab.


Bi Rajab alielezea masikitiko ambayo familia yao inapitia baada ya aliyekuwa wakili wa ndugu yao kujiuzulu.


“Kufikia sasa hatujaarifiwa wakili wake mpya ni nani. Ndugu yangu alipatikana hana hatia na ikasemekana anarudi nchini. Ni matumaini yetu kama familia ya Bw Abdul kuwa Serikali itamzingatia pia yeye na kumrudisha aungane na familia na jamaa zake,” alisema Bi Rajab.


Malik alishutumiwa na Amerika kwa kuendeleza uhusiano wa karibu na wanachama wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda katika Afrika Mashariki na kuwa na uhusiano na wanachama wakuu.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE