Benki ya Uganda yazindua akaunti ya kwanza inayofuata sheria za Kiislamu

 

Benki ya Finance Trust ya Uganda imezindua akaunti ya kwanza kabisa inayofuata sheria za Kiislamu katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.


Viongozi na shakhsia mbalimbali wa Kiislamu walihudhuria hafla ya uzinduzi wa akaunti hiyo inayoitwa 'Halal' jana Alkhamisi katika mji mkuu Kampala.


Julai mwaka huu, Baraza la Mawaziri la Uganda liliidhinisha benki za kibiashara za nchi hiyo kutoa huduma zinazofuata mfumo wa kibenki wa Kiislamu.


Haria Nakawunde, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Finance Trust ya Uganda amesema, akaunti hiyo ya Halal ambayo ni ya kwanza kuzinduliwa rasmi nchini humo, haitawatoza wateja wao riba wanapochukua mikopo.


Naye Hajj Karim Kallisa, mjasiriamali mashuhuri nchini Uganda ambaye alikuwa mgeni wa heshima katika uzinduzi wa jana ameashiria wimbi la kufunguliwa benki na taasisi nyingine za kifedha zinazofuata mafundisho ya Kiislamu katika nchi mbalimbali barani Afrika na kusema: Benki zinazozingatia sheria za Kiislamu sio mahsusi kwa ajili ya Waislamu tu, bali kwa jamii yote ya mwandamu.


Benki za Kiislamu katika nchi jirani za Kenya na Tanzania na vile vile nchini Ethiopia zimeendelea kupata umaarufu na kupongezwa kwa huduma zao, na sasa zinawavutia kwa wingi hata wateja wasiokuwa Waislamu.


Mwezi uliopita wa Septemba, shirika la taarifa za kifedha la Moody's Investors Service lilisema katika ripoti mpya kuwa, rasilimali za benki za Kiislamu barani Afrika zinatarajiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka 10 ijayo, kutokana na idadi kubwa ya Waislamu barani humo.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE