Matumizi Ya Tehama Mahakama Yafikia Asilimia 71

Na Magreth Kinabo – Mahakama
Mwenyekiti wa Kamati ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Takwimu   ya Jaji Mkuu, Mhe. Shaaban   Lila amewataka  wajumbe wa kamati hiyo kutoa uzoefu wao kuhusu matumizi  ya teknolojia na kuzitafutia ufumbuzi changamoto   mbalimbali  wanazokabiliana nazo  katika eneo hilo.

Akizungumza jana wakati akifungua kikao cha kamati hiyo cha siku mbili  kilichofanyika kwenye ukumbi wa mkutano wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi  uliopo Jijini Dar es Salaam, Jaji  Lila, ambaye  pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, alisema teknolojia hiyo imeanza kutumika   mahakamani  na wana majukumu tisa ya kuyafanyia kazi.

‘‘Tutumie kikao hiki kubadilishana uzoefu na kuzitafutia ufumbuzi changamoto tunazokabiliana nazo katika matumizi ya TEHAMA ukitaka kutatua tatizo ni lazima uliweke bayana na kulitafutia ufumbuzi, ’’ alisema Mwenyekiti huyo.

Lila aliongeza kwamba kamati hiyo imepewa majukumu mbalimbali ya kuyatekeleza ili kuhakikisha eneo la  TEHAMA linatekelezwa  ipasavyo,  hivyo aliwataka wajumbe hao kutoa ushauri  wa kuendelea kuboresha eneo hilo.

Alifafanua kuwa  mifumo ya TEHAMA iendelee kuboreshwa  iwe ya manufaa kwa  wananchi na  Mahakama pia kuwataka wajumbe wa kikao hicho kuyataja maeneo yanayotakiwa kuboreshwa.

 Kwa upande wake Katibu wa kamati hiyo, ambaye pia Mkurugenzi wa  TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Enock Kalege akitoa taarifa ya maendeleo ya teknolojia hiyo, alisema  imeleta matokeo chanya  katika shughuli mbalimbali za  Mahakama  licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto kama vile rasilimali fedha na watu   kwa ajili ya kuendelea kulitekeleza jukumu  husika.

 Kalege alisema kwamba teknolojia hiyo pia inasaidia kuwa na takwimu  sahihi kama vile vifaa vya TEHAMA  ili kuweza  kuboresha  na kupanga   mipango ya sasa na baadae kwa faida  ya Mahakama.

‘‘Tumefanikiwa kukamilisha jukumu hili la TEHAMA kwa asilimia 71 kupitia miradi ya uwekezaji kwenye eneo hili, na  tunaendelea  kutekeleza asilimia  29  iliyobakia,’’ alisisitiza.

Akizungumzia kuhusu eneo hilo, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma alisema kwa upande wa kufungua  mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao limeendelea kutekelezwa kama ilivyoagizwa na Jaji Mkuu wa Tanzania.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru alisema ili kuhakikisha teknolojia  hiyo inaendelea kurahisisha huduma ya utoaji haki na kupunguza  gharama za uendeshaji wa shughuli  tofauti  za Mahakama  ni vema watumishi wakaendelea kujengewa uwezo na kubadili mitazamo yao.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE